Ni rahisi kusema Simba wamezidiwa tena ujanja baada ya kipa wanayedaiwa kumtaka Washington Arubi kutoka Marumo Gallants kusaini mkataba wa kuichezea timu nyingine.
Arubi alionyesha kiwango cha juu wakati Marumo Gallants walipovaana na Yanga kwenye hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kuelezwa kuwa Simba walionyesha nia ya kumsajili.
Chanzo cha uhakika kutoka ndani ya Simba kimeeleza kuwa, jina la kipa huyo lilikuwa mezani kwa kocha Robert Olivier Robertinho likijadiliwa, lakini amepata taarifa kuwa ameshasaini dili jipya la kukipiga sehemu nyingine.
Taarifa iliyoripotiwa na magazeti ya Afrika Kusini inasema kuwa kipa huyo ambaye pia alikuwa akiwindwa na Simba ameshasaini mkataba wa mwaka mmoja kwenye kikosi cha Sekhukhune United ya huko.
Arubi ameondoka Marumo bure kwa kuwa mkataba wake umeshamalizika na sasa ataitumikia timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu Afrika Kusini kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.
Kipa huyo alikuwa na kipindi kizuri ndani ya Marumo Gallants na mwishoni mwa msimu alikuwa mmoja kati ya wachezaji waliopewa tuzo kutokana na mchango mkubwa kwenye timu hiyo ambayo imeshuka daraja.
Kwa mujibu wa taarifa, Simba walikuwa wanamhitaji kipa huyo raia wa Zimbabwe ili awe msaidizi wa Aishi Manula ambaye kwa sasa yupo Afrika Kusini na tayari ameshafanyiwa upasuaji wa nyama za paja.
Hii ni mara ya pili mchezaji anayetakiwa na Simba kusajiliwa na timu nyingine baada awali kuelezwa kuwa beki Yahya Mbegu wa Ihefu aliyekuwa anatakiwa na timu hiyo naye amechukuliwa juu kwa juu na Singida Big Stars.
Vilevile wakati wa dirisha dogo la usajili Januari, mwaka huu, Wekundu hao walihusishwa na Mudathiri Yahya, lakini akatua Young Africans.