Imefahamika kuwa Uongozi wa Simba SC, umegomea ofa kutoka Klabu ya Gor Mahia ya nchini Kenya ambayo imeonesha nia ya kumuhitaji beki wa timu hiyo, Joash Onyango.

Ofa hiyo inadaiwa kutua Msimbazi, baada ya siku chache tangu tetesi zizagae kumuhusu beki huyo raia wa Kenya, ambaye alidaiwa kuandika barua ya kuomba kuondoka Simba SC mwishoni mwa msimu huu.

Taarifa kutoka Kenya zinaeleleza kuwa klabu ya Gor Mahia inayoshiriki Ligi Kuu nchini humo, imewasilisha ofa hiyo, hivi karibuni ikiomba huduma ya beki huyo kwa ajili ya msimu ujao 2023/24.

Mtoa taarifa hizi amesema, ofa hiyo imekataliwa na mabosi wa Simba SC, wakidai ni ndogo, huku wakiitaka Gor Mahia iongeze fedha ili wakamilishe dili hilo.

Ameongeza kuwa, Simba SC wapo tayari kumuachia beki huyo, kama makubaliano yatafikia sehemu nzuri kwani tayari wapo katika mazungumzo na mabeki waliopanga kuwasajili.

“Gor Mahia ya nchini Kenya imeonesha nia ya kutaka kumsajili Onyango kwa ajili ya msimu ujao, lakini Simba imegoma ikitaka iongezewe pesa na sio hiyo ofa ndogo waliowekewa mezani.

“Simba SC ipo tayari kumuachia Onyango kuondoka ila kwa timu itakayofika dau wanalolihitaji kama uongozi utafikia makubaliano mazuri.

“Bado mazungumzo yanaendelea kati ya uongozi wa Gor Mahia na Simba SC, kama makubaliano yakifikia pazuri, basi beki huyo hatakuwa sehemu ya wachezaji wetu msimu ujao,” amesema mtoa taarifa huyo.

Akizungumzia hilo, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, amesema kuwa: “Uongozi hivi sasa unafanya vikao pamoja na kocha Robertinho (Roberto Oliviera) kwa ajili kuweka mikakati ya usajili, kikubwa tumepanga kufanya usajili mkubwa utakaoendana na klabu yetu ambao utatufikisha Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.”

Granit Xhaka kuondoka Arsenal
Wakulima zingatieni maelekezo ya maafisa ugani - Serikali