Mshambuliaji wa Tottenham Hotspurs, Harry Kane huenda akarejea uwanjani wakati wa mchezo wa ligi ya nchini England dhidi ya mahasimu wao wa jijini London, Arsenal.
Mshambuliaji huyo ameibua mashaka ya kuukosa mchezo huo muhimu kufuatia majeraha ya mguu aliyoyapata wakati wa mchezo wa robo fainali ya kombe la FA dhidi ya Milwall, uliochezwa mwishoni mwa juma lililopita kwenye uwanja wa White Hart Lane.
Spurs walitoa taarifa za majibu ya Kane usiku wa kuamkia leo baada ya kufanyiwa vipimo jana mchana, na imebainika alijitonesha jeraha la kifundo cha mguu ambalo lilimuweka nje mwanzoni mwa msimu huu.
Jopo la madaktari la klabu hiyo limeuthibitishia uongozi wa klabu hiyo ya kaskazini mwa jijini London kuwa Kane anaweza kuuwahi mchezo dhidi ya Arsenal ambao umepangwa kuchezwa April Mosi katika uwanja wa White Hart Lane.
Kwa upande wa Kane aliwaeleza mashabiki wake kupitia Twitter, “Sitoweza kucheza kwa siku za karibuni, naamini nitakaporejea uwanjani, nitakuwa na nguvu zaidi. Ninawashukuru wale wote walionitakia pole.”