Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemuagiza Waziri wa Madini, Dkt. Dotto Biteko afuatilie taasisi za fedha zinazowakopesha wachimbaji wadogo kwa kuangalia viwango vya riba vinavyotolewa na aina ya shughuli wanazozifanya wajasiriamali hao, ili kurahisisha urejeshwaji wa mikopo.
Majaliwa ameyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Salome Makamba katika kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu Bungeni Jijini Dodoma. Mbunge huyo alitaka kufahamu Serikali ina mpango gani wa kutengeneza mazingira rafiki ya upatikanaji wa mikopo kwa wachimbaji wadogo kulingana na uhalisia wa biashara zao.
Amesema Serikali inatambua changamoto ya masharti mbalimbali kwa taasisi za kifedha, hivyo imetoa maelekezo kwa taasisi hizo kuwa zitambue aina ya shughuli zinazofanywa na wajasiriamali hao na muda unaotumika kuanzia uwekezaji hadi uzalishaji wake ili masharti yaendane na shughuli husika.
Pia, Waziri Mkuu amewashauri wajasiriamali hao wajiunge katika vikundi ili waweze kupata mikopo inayotolewa na Serikali (asilimia 10 ya mapato ya halmashari), mifuko ya uwezeshaji pamoja na inayotolewa na taasisi mbalimbali za kifedha.