Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imekamillisha kumchunguza aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Deusdedit Kakoko.
Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo amesema kuwa taasisi hiyo imekamilisha kwa asilimia 98 uchunguzi dhidi ya Kakoko na maafisa wengine wa TPA. Amesema wanasubiri Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Dkt. Charles Kichere ili wakamilishe kwa asilimia 100.
“Asilimia mbili zilizobakia ni taarifa ya CAG ambayo ni muhimu sana, bila hiyo hatuwezi kwenda mahakamani,” amesema Brigedia Jenerali Mbungo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan aliiagiza taasisi hiyo kumchunguza Kakoko baada ya kumsimamisha, kufuatia tuhuma za ufisadi na matumizi mabaya ya ofisi.
Uchunguzi huo ulilenga kutambua zaidi ya Shilingi bilioni 3.6 zilivyotumika katika bandari hiyo, kufuatia ripoti ya CAG.
Siku mbili baada ya maagizo ya Rais Samia, Takukuru ilimkamata Kakoko na kumhoji kutokana na tuhuma hizo. Pia, ilifanya upekuzi katika nyumba yake.