Tanzania imejitolea kuzuia na kupambana na Biashara Haramu ya Usafirishaji Binadamu kwa kuhakikisha inatambua na kushughulikia mambo mbalimbali ya kijamii, kiuchumi, kiutamaduni na kisiasa ambayo yanawafanya watu kuwa hatarini na kuhusika katika biashara hiyo haramu.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango hii leo Januari 30, 2023 jijini Dar es Salaam wakati akifungua Kongamano la Mashauriano la Maaskofu, Wachungaji na Viongozi Wakuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania na Mataifa mengine duniani kuhusu kupiga vita Biashara Haramu ya Usafirishaji Binadamu.
Amesema, “Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na wadau wengine inaendelea kuchukua hatua madhubuti ili kuharakisha ukuaji wa uchumi, kupunguza umaskini, na kuboresha ustawi wa kijamii na kiuchumi wa wananchi ili kuwaepusha na kadhia ya biashara hiyo.”
Aidha, Makamu wa Rais ameongeza kuwa ili kukabiliana na usafirishaji haramu wa binadamu, serikali imeendelea kujenga taasisi imara ili kurahisisha upelelezi na uendeshaji wa kesi za kadia hiyo pamoja na kutunga sheria ikiwa ni pamoja na Sheria ya Kupambana na Biashara Haramu ya Usafirishaji Binadamu ya mwaka 2008.