Jeshi la Polisi nchini, limewataka wafugaji wote nchini kuacha mara moja tabia ya kuhamisha mifugo kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine bila ya kufuata utaratibu wa kupata vibali toka serikalini kwani jeshi hilo halitaruhusu jambo hilo kutokea na litachukua hatua kwa kukamata mifugo hiyo.

Hatua hiyo, inatokana na kikosi cha Kuzuia Wizi wa Mifugo (STPU), kupitia operesheni mbalimbali kufanikiwa kukamata jumla ya mifugo 2,225 ambayo iliyokua inasafirishwa bila kufuata utaratibu na iliyoingizwa katika mapori tengefu pamoja na vyanzo vya maji.

Kamanda wa Polisi Kikosi cha Kuzuia Wizi wa Mifugo Nchini, Kamishna Msaidizi wa Polisi. Simon Pasua kupitia taarifa yake amesema operesheni hiyo iliyofanyika mwezi huu ambapo watuhumiwa 48 walikamatwa wakiwa na mifugo hiyo kwa makosa mbalimbali.

Amesema, “kati ya mifugo iliyokamatwa 1,263 ilikamatwa katika pori tengefu la Pololeti wilayani Ngorongoro na 962 ilikamatwa ikisafirishwa kutoka Mkoa wa Morogoro kwenda mkoa wa Ruvuma bila ya kufuata taratibu za kisheria.”

Aidha, Kamanda Pasua ameyataja makosa hayo kuwa ni pamoja na kuingiza mifugo katika vyanzo vya maji, kusafirisha kutoka mkoa mmoja kwenda Mkoa mwingine bila kuwa na kibali na kuingiza mifugo kiholela katika mapori tengefu ama vyanzo vya maji.

Tanzania kupambana na biashara ya usafirishaji Binadamu
Azaki waaswa kushirikiana na Halmashauri, jamii