Beki na Nahodha wa Kikosi cha Tanzania Prisons, Jumanne Elifadhili, ameweka wazi kuwa, akili zao zote kwa sasa ni kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Namungo FC.
Timu hiyo imetoka kupoteza mchezo wa Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ Hatua ya 16 Bora dhidi ya Young Africans kwa kufungwa mabao 4-1, Ijumaa (Machi 03) na kuondolewa mashindanoni.
Elfadhili ambaye ndiye alifunga bao pekee kwa timu yake katika kipigo hicho walichokipata Uwanja wa Azam Complex, Dar, amesema kwa sasa akili zao ni kwenye mchezo dhidi ya Namungo.
“Kwa sasa akili zetu ni kwenye mechi dhidi ya Namungo ambayo hiyo ni ya ligi. imekuwa hivyo kutokana na nafasi yetu ambayo tupo, hivyo tutapambana kupata ushindi.” amesema Elfadhili
Machi 11, mwaka huu, Tanzania Prisons itakuwa na kibarua cha kusaka alama tatu kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara ugenini dhidi ya Namungo utakaochezwa Uwanja wa Majaliwa, Lindi.
Katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, Prisons inashika nafasi ya 14 ikiwa na alama 22, Namungo wana alama 32, zote zikiwa zimecheza mechi 24.