Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeteuliwa kuwa miongoni mwa nchi tisa za wajumbe wanaounda kamati ya hati za utambulisho ya Baraza kuu la umoja wa mataifa.
Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Profesa Gaston Kennedy amesema kazi kubwa ya kamati hiyo ni kupitia na kujiridhisha juu ya hati zote za wawakilishi wa nchi wanachama wa umoja wa mataifa walioteuliwa na baraza hilo.
Amesema kuteuliwa kwa Tanzania katika kamati hiyo ni ishara nyingine inayoonyesha namna ambavyo umoja wa mataifa una imani na Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli na pia nchi wanachama wanavyoiamini katika kutekeleza misingi mikubwa ikiwemo masuala ya usalama, haki za binadamu na utawala bora.
Hii ni mara ya tatu kwa Tanzania kuteuliwa kuingia katika kamati hiyo ambapo kwa mara ya kwanza iliteuliwa katika baraza la 64 mwaka 2009, mara ya pili baraza la 69 mwaka 2013, na mara ya tatu ni mwaka huu 2020.
Nchi nyingine zilizoteuliwa ni Cameroon, Iceland, Papua New Guinea, Urusi, Tobago, Marekani na Uruguay.