Katika harakati za kuwawezesha wanawake ili waweze kufanya shughuli zao za kimaendeleo, Kampuni ya Tanzanite One, imetoa msaada wa Sh. 20 milioni kwa chama cha Madalali wanawake,wanaouza madini ya Tanzanite mkoani Arusha .

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa kampuni hiyo, inayomilikiwa kwa pamoja na kampuni ya Sky Associate Ltd na shirika la madini la taifa(STAMICO), Faisal Shabhai.

Amesema kuwa wamefikia uamuzi wa kutangaza hatua hiyo mara baada ya kufanya mazungumzo na madalali hao wanawake jijini Arusha.

Faisal amesema kuwa Kampuni yao ambayo inachimba Tanzanite, imetoa msaada wa sh. 20 milioni, ili kuendelea kutekeleza mahusiano mema na wadau wa Tanzanite na jamii ya wanawake ambao wanajihusisha na biashara ya kuuza madini hayo.

Aidha, ameongeza kuwa msaada huo, umetokana na maombi ya wanawake hao, kusaidiwa waliyoyatoa katika mkutano na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo na viongozi wa Tanzanite One.

Katika hatua nyingine Kampuni hiyo imetenga kiasi cha sh. 200 milioni kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa hospitali ya kisasa Mererani.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa chama hicho, Eugen Augustine amesema kuwa madalali wa madini wanawake mkoani Arusha, wanakabiliwa na tatizo la mtaji mdogo na hivyo kushindwa kujiendesha na kunufaika na biashara yao.

Katika hatua nyingine, Kampuni hiyo, imetoa msaada wa mahindi  magunia 250 kwa wananchi wakazi wa kata ya Naisinyai ikiwa ni sehemu ya mchango wa kampuni hiyo kwa jamii inayozunguka migodi yake.

Hata hivyo, Faisal amesema kuwa msaada huo, utasaidia makundi maalum katika jamii na ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipoishauri kampuni hiyo kutoa misaada mara kwa mara kwa jamii inayowazunguka.

 

Majaliwa amwakilisha Rais Dkt. Magufuli uzinduzi Jukwaa la Uchumi
Steve Nyerere: Nilitumia ujasiri wa kiume kuomba radhi hadharani