Balozi wa Tanzania nchini Uturuki, Luteni Jenerali Mstaafu Yacoub Mohamed amewataka Watanzania walio na ndugu zao nchini Uturuki kufanya mawasiliano kujua hali zao kisha kutoa taarifa endapo kuna madhara ili waweze kuchukua hatua, baada ya kutokea kwa tetemeko la ardhi lililosababisha vifo zaidi ya watu 1,000 nchini humo.
Balozi Mohamed ameyasema hayo hii leo Februari 7, 2023 wakati akifanya mahojiano na Mwandishi wa shirika la Utangazaji nchini – TBC na kusema hadi kufikia sasa kwa Watanzania waliowasiliana nao hali zao ni shwari na kwamba kama kuna yeyote ambaye ana taarifa za ziada anatakiwa kuziwasilisha ili zifanyiwe kazi.
Tukio hilo la tetemeko la ardhi la ukubwa wa 7.8 kwa kipimo cha richa, ambalo limezikumba nchi za Uturuki na Syria limesababisha majeruhi na vifo vingi, ambapo idadi ya waliofariki inaendelea kuongezeka kwani tayari Watu 2,921 wameripotiwa kufariki Nchini Uturuki huku zaidi ya 15,000 wakijeruhiwa.
Kwa upande wa Syria, ripoti zinasema waliofariki ni 1,444 ikifanya jumla ya vifo kufikia 4,365 na idadi hiyo ya vifo inatarajiwa kuongezeka huku Rais wa Korea Kusini, Yoon Suk-yeol akisema nchi yake itatuma timu ya waokoaji na vifaa vya matibabu ya dharura kwenda Uturuki kusaidia shughuli za uokoaji.