Taarifa zinaeleza kuwa huenda Mkataba wa Mkopo kati ya Simba SC na TP Mazembe unaomuhusu Mshambuliaji Jean Baleke ukavunjwa mwishoni mwa msimu huu, kuafuatia miamba hiyo ya Lubumbashi kupokea ofa kutoka moja ya klabu za Barani Ulaya.
Baleke anaewika Simba SC kwa sasa alisajiliwa kwa mkopo wa miaka miwili mwezi Januari 2023, baada ya kugoma kuitumikia TP Mazembe akitokea nchini Lebabon ambako alipelekwa kwa mkopo wa miezi sita mwanzoni mwa msimu huu.
Taarifa hizo zinaeleza kuwa TP Mazembe tayari wameiarifu Simba SC ili wakae mezani kwa ajili ya kuvunjwa kwa mkataba wa mkopo wa Mshambuliaji huyo, ili kutoa nafasi kufanywa kwa biashara ya kuuzwa kwa Baleke katika klabu hiyo ya Ulaya ambayo inatajwa kuwa kwenye nafasi nzuri ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Barani humo msimu ujao 2023/24.
Endapo makubaliano ya kuvunjwa kwa mkataba wa mkopo baina ya pande hizo mbili yatafikiwa kikamilifu, Baleke atakuwa na nafasi kubwa ya kuondoka Simba SC mwishoni mwa msimu huu, kwa ajili ya kwenda kuanza maisha mapya huko Barani Ulaya.
Hata hivyo taarifa hizo zinakwenda kinyume na Meneja wa Beleke ambaye aliwahi kusema Simba SC inaangalia uwezekano wa kumsajili moja kwa moja Mchezaji wake ambaye alisaini mkataba wa miaka mitano na TP Mazembe.
Meneja huyo alithibitisha kuwa Samba SC imemsajili Baleke kwa mkopo wa Miaka miwili huku Mshambuliaji huyo akiwa tayari ameshaitumikia TP Mazembe kwa miaka miwili, hivyo kilichokuwa kinaendelea ni kununuliwa kwa mkataba wa mwaka mmoja unaosalia, ili wanyakue jumla jumla.