Aliyekua kocha mkuu wa Taifa Stars Emmanuel Amuneke amewasilisha malalamiko kwenye shirikisho la soka duniani FIFA, dhidi ya shirikisho la soka Tanzania TFF.
Kocha huyo kutoka nchini Nigeria, anaendelea kukumbukwa kwa mafanikio ya kuiwezesha Taifa Stars kufuzu fainali za mataifa ya Afrika 2019 baada ya miaka 40, amefanya hivyo na kuthibitisha kwa waandishi wa habari, huku akisema sababu kubwa ni kutolipwa stahiki zake.
Amunike amesema hakutendewa haki na uongozi wa TFF, baada ya kuvunjiiwa mkataba wake siku chache baada ya Taifa Stars kuondolewa kwenye fainali za Afrika, zilizounguruma nchini Misri kati ya Juni 21 hadi Julai 19.
Kocha huyo ambaye aliwahi kuitumikia timu ya taifa ya Nigeria kama mchezaji kwa mafanikio makubwa mwaka 1994 na kutwaa taji la Afrika, amesema amewasisha malalamiko yake FIFA, na anaamini haki itatendeka.
“Ninaamini mlalamiko yangu yatasikilizwa, na haki itatendeka, sikufanyiwa jambo zuri na viongozi wa soka la Tanzania, sio sahihi mtu kutolipwa stahiki zake baada ya kufanya kazi,” alisema Amuneke.
TFF ilivunja makataba wa kocha huyo, baada ya Taifa Stars kufanya vibaya katika fainali Afrika kwa kupoteza michezo yote ya hatua ya makundi.
Taifa Stars ilianza fainali hizo kwa kufungwa na Senegal mabao mawili kwa sifuri, kisha ikafungwa na Kenya mabao matatu kwa mawili na baade Algeria wakaibuka na ushindi wa mabao matatu kwa sifuri.