Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania – TMA, imesema inafuatilia mifumo ya hali ya hewa kuhusu kunyesha kwa mvua za El Nino kutokana na uwepo wa uwezekano wa kunyesha mvua hizo kwa asilimia 60.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya Habari, TMA imeeleza kuwa imekuwa ikifuatilia mifumo ya hali ya hewa wakati wa maandalizi ya msimu wa mvua za masika kwa mwezi Machi – Mei, 2023 ikiwemo mvua za El Nino.
Imesema, hatua hiyo inatokana na taarifa ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa – FAO, iliyotahadharisha pia uwezekano wa kunyesha kwa mvua hizo katika nchi za Afrika upande wa Mashariki na Kusini.
Mvua hizo kwa mara ya mwisho zilinyesha mwaka 2016 hapa nchini na kusababisha madhara yakiwemo mafuriko ambapo maeneo ya Kaskazini, Pwani ya Kaskazini ya mikoa ya Pwani, Kaskazini mwa mikoa ya Morogoro, Dar es Salaam, Tanga na visiwa na Unguja inaweza kuathiriwa.