Rais wa Marekani, Donald Trump ameliagiza Jarida la New York Times kumfichua afisa wa serikali yake, aliyeandika makala ya gazeti hilo, akidai kuwa baadhi ya wafanyakazi serikalini walikuwa wakifanya kila wawezalo ili kukwamisha ajenda yake ya maendeleo.
Trump amemtaja mwandishi wa makala hiyo, ambaye jina lake limehifadhiwa, kama mchochezi, na kusema kuwa uchapishaji wa makala hiyo ni kosa la jinai.
Mwandishi huyo ambaye jina lake limehifadhiwa alisifu kidogo ufanisi wa utawala wa Trump, lakini akasema baadhi ya maamuzi ya rais huyo yamekuwa yasiyofikirika na ya kipuuzi.
Aidha, Msemaji wa Jarida la New York Times amesema kuwa gazeti hilo linajivunia kuwa lilichapisha makala hiyo, ambayo amesema kuwa imesaidia raia kuelewa kile kinachoendelea katika uongozi wa Rais Trump.
Hata hivyo, rais Trump amelikosoa Jarida la The New York Times kwa kuchapisha makala hiyo, huku akisema kuwa makampnui yote ya habari yatakosa biashara mara atakapoondoka ofisini kwakuwa hayatakuwa na kitu cha kuandika tena.