Mkutano wa kilele wa kundi la mataifa yaliyoendelea na yale yanayoinukia kiuchumi G20 unaanza leo Jumamosi chini ya mwenyeji Saudi Arabia, ukigubikwa na wingu la janga la virusi vya Corona.
Shughuli za mkutano huo wa kilele ambao kwa kawaida huwakutanisha ana kwa ana viongozi wa madola yenye nguvu, zimepunguzwa na badala yake kutakuwa na majadiliano mafupi kupitia njia ya video kuhusu masuala yanayokabili ulimwengu, hasa athari za janga la virusi vya Corona.
Taarifa ambazo zimethibitishwa na afisa wa ngazi ya juu wa serikali ya Marekani zimeeleza kuwa Rais wa Marekani Donald Trump, atakuwa sehemu ya viongozi watakoshiriki mkutano huo wa kilele wa kundi la G20.
Mbali na athari za Corona, Mkutano huo pia utajadili kuhusu mabadiliko ya tabia nchi na kuongezeka kwa ukosefu wa usawa duniani.
Saudi Arabia ambayo ndiyo mwenyeji wa mkutano huo wa siku mbili, imekuwa nchi ya kwanza ya kiarabu kuandaa Mkutano wa G20.
- G20 yarefusha muda wa mataifa masikini kulipa madeni
- WB, IMF wawaomba G20 kuzisamehe madeni nchi masikini