Rais wa Marekani, Donald Trump na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu wameungana kuzionya nchi za Korea Kaskazini kuachana na mipango yao ya makombora ya maangamizi ili wasiziharibu.
Viongozi hao wa mataifa yenye historia kubwa ya urafiki walitoa kauli hizo jana walipokuwa wakihutubia katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa.
Katika hotuba yake, Rais Trump alieleza kuwa Marekani itaiharibu na kuisambaratisha Korea Kaskazini kama itaendelea na mpango wake wa majaribio ya makombora ya nyuklia. Alisema nchi yake ina nguvu na uwezo wa kufanya hivyo.
“Marekani itaiharibu kabisa Korea Kaskazini kama itaendelea na mpango wake. nina uwezo wa kufanya hivyo wakati wowote, kama italazimika kufanya hivyo,” alisema na kuongeza kuwa kiburi cha kiongozi wa Korea Kaskazini ni sawa na mpango wa kutaka kujiua.
Katika hatua nyingine, Trump alikosoa vikali mazungumzo kati ya Marekani na Iran kuhusu mpango wa Nyuklia (Iran nuclear deal) ulioratibiwa na watangulizi wao akieleza kuwa ni mpango wa kughafirisha kwa Marekani.
Aidha, Trump aliitaka Iran kuacha mara moja kufadhili vitendo vya kigaidi na kwamba nchi hiyo inajaribu kuvuruga amani ya Mashariki ya Kati.
Kwa upande wa Netanyahu ambaye alieleza kuunga mkono hotuba yote ya Trump iliyojaa vitisho dhidi ya Korea Kaskazini na Iran, alisema kuwa Serikali ya Iran ni adui mkubwa wa nchi yake.
Alisema mpango wa Iran wa nyuklia umelenga katika kutaka kuishambulia Israel hivyo hatakubali kuona ukiendelea.
“Wananchi wa Iran ni marafiki zetu, sio maadui. Lakini Serikali kandamizi na ya kidikteta ya Iran ni adui yetu mkubwa na sisi hatutakubali kuona inaendelea na mpango wake wa nyuklia kwa lengo la kutushambulia,” alisema.
“Naunga mkono hotuba ya Rais Trump. Amesema ukweli mtupu, ameuita mpango wa mazungumzo ya nchi yake na Iran kuwa ni mpango unaoghafirisha,” aliongeza.
Viongozi hao kwa pamoja walieleza Iran na Korea Kaskazini sio tu ni tishio kwa usalama wa nchi zao bali kwa usalama wa dunia nzima.