Nahodha na kiungo Young Africans, Papy Kabamba Tshishimbi amewaambia mashabiki wa klabu hiyo kuwa, kuna uwezekano mkubwa wa mshambuliaji wa FC Lupopo ya DR Congo Mpiana Mozizi kutua Jangwani kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kuu.

Tshishimbi amepata ujasiri wa kuwaarifu mashabiki wa Young Africans taarifa hizo, baada ya kuzungumza kwa njia ya simu na mshambuliaji huyo, na kumthibitishia uwezekano wa kusajiliwa klabuni hapo.

Kiungo huyo amesema Mpiana amemwambia anaendelea kushawishika kujiunga na Young Africans baada ya kuongea na mabosi wawili wa klabu hiyo kongwe hapa nchini akiwamo Mhandisi Hersi Said, na kigogo mwingine ambaye yupo nje ya uongozi lakini mwenye ushawishi mkubwa.

“Amenipigia juzi tu hapa nimeongea kwa muda wa kutosha tu ameniambia anataka kuja hapa Young Africans na sio klabu nyingine, sasa kuna mambo alitaka kujua kwanza juu ya timu yetu na nimemweleza amekubali ameniambia anakuja hapa,” amesema Tshishimbi

“Mpiana ni mshambuliaji bora sana kama atakuja hapa nafikiri tangu niijue Young Africans ndio watafurahi kuona kazi ya mshambuliaji halisi anayejua kupambana na kufunga ndio maana anaongoza kule Congo,”

“Mpaka ligi ya Congo inasimama alikuwa na mabao 12, akifungana na Jackson Muleka wa TP Mazembe na Fiston Mayele wa AS Vita.

Tshishimbi amesema mchezaji huyo alimdokeza pia, alishapata ofa ya Simba lakini sasa akili yake ameihamishia Young Africans ambapo anaona wako makini katika harakati za kumsajili.

“Unajua nimekuwa nikiwashauri sana viongozi kuna wachezaji wazuri sana sehemu mbalimbali sasa kila nikiona kuna upungufu sehemu huwa nasema. Msimu huu na hata ule tulipata shida katika kufunga sana, sasa tunahitaji watu bora kama alivyo Mpiana kule mbele tunatakiwa kuwa na nguvu, naamini kwa viongozi ambao Mpiana amenitajia anawasiliana nao basi hakuna shaka watamleta akija watu wa Young Africans watafurahi,” alisema Tshitshimbi.

Baadhi ya mataifa kulegeza masharti ya kukabiliana na Corona
Gharama za kutengeneza ‘dawa’ maabara zawekwa wazi