Naibu Waziri, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi-Sekta ya Uchukuzi, Atupele Mwakibete ametoa wito kwa wadau kutumia vyema taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na Mamlaka kwa ajili ya kupanga shughuli za kijamii na kiuchumi pamoja na kufanya maamuzi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Mwakibete ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu siku ya kimataifa ya hali ya hewa Duniani, na kuongeza kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi 193 wanachama wa WMO ambayo imeungana na Jumuiya ya Kimataifa kuadhimisha miaka 73 ya WMO na maadhimisho ya miaka 150 ya Shirika la Kwanza la Kimataifa la Hali ya Hewa.
Amesema, katika kuhakikisha kunakuwa na taarifa za uhakika za hali ya hewa Serikali nchini imefanya uwekezaji katika huduma za hali ya hewa, ikiwemo ununuzi wa miundombinu ya kisasa ya uchunguzi wa hali ya hewa ikiwa ni pamoja na Rada za hali ya hewa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi sehemu ya ajali za ndege wizara ya ujenzi na uchukuzi, Redemptus Bugomola amevitaka vyombo vya Habari kutoa taarifa sahihi kuhusiana na ajali ya Ndege iliyotokea Mkoani Kagera hivi karibuni, na badala yake kuiachia mamlaka husika kutoa taarifa sahihi.