Baadhi ya Wafanyabiashara jijini Dar es Salaam, wamesema wanasubiri kwa hamu majibu ya kamati iliyoundwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa juu ya kushughulikia kero mbalimbali walizoziainisha kwenye kikao cha pamoja.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Wafanyabiashara hao wengi walisema endapo Serikali itajumuisha maoni yao bila walakini na kufanyia kazi kwa haki na kwa kusimamia misingi ya kisheria na taratibu wana matumaini kuwa suala la kukuza pato la Taifa na mtu mmoja mmoja litafanikiwa tofauti na ilivyo sasa ambapo kuna mianya mingi ya rushwa
Hatua hiyo inajiri huku ikiwa tayari Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan akifanya Kikao Maalum na Watendaji mbalimbali wa Wizara ya Fedha na Mipango wakiongozwa na Waziri wake Dkt. Mwigulu Nchemba, hapo jana Mei 18, 2023.
Kikao hicho kilichofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, pia kilishirikisha Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara wakiongozwa na Waziri wake Dkt. Ashatu Kijaji, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakiongozwa na Kamishna Mkuu Alphayo Kidata pamoja na Katibu Mkuu Kiongozi Dkt. Moses Kusiluka.