Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa uliotolewa na aliyewahi kuwa Mbunge wa Butiama mkoani Mara, Marehemu Wakili Nimroad Mkono na kwamba itaendelea kumuenzi kwa kazi nzuri alizofanya.
Majaliwa ameyasema hayo alipomuwakilisha Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika shughuli ya kumuaga marehemu Wakili Nimrod Mkono iliyofanyika kwenye viwanja vya Karimjee, Jijini Dar es Salaam.
Amesema, “Serikali imepoteza mtu muhimu, itaendelea kutambua mchango alioutoa na itaendelea kuyaenzi yale yote mema aliyoyafanya enzi za uhai wake. Wananchi kila mmoja kwa imani yake tuendelee kumuombea.”
Aidha ameongeza kuwa, enzi za uhai wake marehemu Wakili Mkono alikuwa mtumishi mwema na mshauri mzuri kwa Serikali hasa katika sekta ya sheria pamoja na kuishauri namna bora ya kutunga sheria na kanuni zake kupitia Bunge.
Kwa upande wake, Dkt. Harisson Mwakyembe amesema Wakili Mkono alikuwa ni taasisi katika uwakili kutokana na ubunifu mkubwa aliokuwa nao katika kukuza huduma za kisheria na ameacha alama kubwa.
Nimrod Mkono, alizaliwa Agosti 18, 1943 katika kijiji cha Busegwe Kata ya Busegwe na anatarajiwa kuzikwa Mei 29 kijijini Kigori wilayani Butiama mkoani Mara na alifariki Aprili 18, 2023 nchini Marekani alikokuwa akipatiwa matibabu.