Aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu amezungumzia uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kutupilia mbali kesi ya kupinga kuvuliwa ubunge ikieleza kuwa haina mamlaka ya kuisikiliza.
Akitoa uamuzi wa Mahakama hiyo jana, Septemba 9, 2019, Jaji Sirillius Matupa akieleza kuwa kesi hiyo ni ya Kikatiba hivyo inapaswa kufunguliwa kwa mfumo wa kesi ya uchaguzi na si kwa mfumo ambao alikuwa ameutumia mlalamikaji.
Lissu ambaye hivi sasa yuko nchini Ubelgiji, amesema kuwa hakuridhishwa na uamuzi uliotolewa na Jaji kwani yeye hana mgogoro na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, hivyo hapaswi kufuata utaratibu wa kiuchaguzi.
“Nadhani Jaji alikosea, mimi sina mgogoro wowote na Tume ya Taifa ya Uchaguzi au yule Mbunge aliyechaguliwa sasa [Miraji Mtaturu], mimi nina mgororo na yule aliyetangaza kunivua ubunge wangu,” alisema Lissu.
“Endapo Mahakama ingeridhia kuwa nilivuliwa ubunge wangu kimakosa, ina maana kuwa hata ubunge wa aliyopo hivi sasa ungekuwa ni batili, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi hawezi kumkatalia Spika [Job Ndugai] akishamuandikia barua kuwa jimbo lile liko wazi,” aliongeza.
Alisema kuwa safari yake ya kudai ubunge inaendelea na kwamba ataenda katika Mahakama ya Rufaa ambayo ndiyo ya juu zaidi.
Spika Ndugai alitangaza kumvua Lissu ubunge miezi miwili iliyopita akieleza kuwa hakuhudhuria mikutano mitatu ya Bunge bila kutoa taarifa rasmi kwake, na kwamba alikuwa hafahamu alipo bali anamuona kwenye vyombo vya habari akisafiri katika nchi za Magharibi na Ulaya.
Kwa mujibu wa Katiba, kutohudhuria mikutano mitatu ya Bunge bila kutoa taarifa ni moja kati ya sababu za mbunge kukosa sifa za kuendelea kuwa mbunge.
Lissu yuko nchini Ubelgiji akipatiwa matibabu kufuatia majeraha aliyoyapata baada ya kushambuliwa kwa risasi Septemba 7, 2017 jijini Dodoma.