Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu huenda akafutiwa dhamana yake baada ya kutohudhuria jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kusikiliza kesi dhidi yake bila kutoa taarifa yoyote.

Lissu na mhariri wa gazeti la Mawio, Simon Mkina wanakabiliwa na mashtaka ya uchapishaji wa taarifa za uchochezi katika gazeti hilo, Januari 14 mwaka huu.

Hakimu Mkazi, Thomas Simba alimtaka Lissu kufika mahakamani hapo leo huku akieleza kuwa anaweza kuondolewa dhamana yake endapo hatatoa sababu za kuridhisha kuhusu kutohudhuria kwake mahakamani.

“Ninamtaka mshtakiwa [Tundu Lissu] pamoja na wenzake kufika hapa Mahakamani kesho kujieleza ni kwanini dhamana yake isifutwe kwa kushindwa kufika Mahakamani bila kutoa taarifa yoyote,” alisema Hakimu Simba.

Katika hatua nyingine, upande wa Mashtaka ulifanikiwa kuishawishi mahakama kuongeza mashtaka mengine dhidi ya Lissu baada ya kuyafanyia marekebisho kutokana na kutupiliwa mbali na mahakama hiyo hapo awali kutokana na makosa ya kiufundi. Ingawa wakili wa Lissu, Peter Kibatala alipinga uamuzi huo, Hakimu alieleza kuwa ni haki ya upande wa mashtaka kufanyia marekebisho makosa ya kiufundi ya awali.

Hata hivyo, kibatala aliiambia Mahakama kuwa watakata rufaa dhidi ya maamuzi hayo ya kukubaliwa kuongeza mashtaka yaliyokataliwa awali, kutokana na kutoridhishwa nayo huku wakiiomba mahakama kuwapa nakala ya uamuzi huo ili waweze kuandaa rufani yao.

Video: Waziri Mkuu apokea michango ya sh. milioni 40, Waathirika Kagera
Marekani Yalaani Shambulio lililotokea nchini Syria