Rais Samia Suluhu Hassan hii leo tarehe 27 Oktoba 2021, amewakabidhi hati za viwanja Wachezaji wote wa timu ya Taifa ya wanawake Tanzania, Twiga Stars.

Rais Samia amefanya tukio hilo wakati wa hafla fupi iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam ya kuwapongeza Timu hiyo kwa ushindi wao katika kombe la COSAFA pamoja na kuwapongeza warembo walioshiriki mashindano ya Viziwi na kufanikiwa kushika nafasi ya pili Afrika.

“Nimeamua kuwapa viwanja hivi kule ninakoishi mimi Dodoma ili tukae wanawake karibu, japo kwenu mtaona mbali na labda wengine watashindwa kujenga kule ila najua umri wenu wote mtaumalizia kwenye kazi hii ya mpira na vijisenti vyenu mnavimalizia kwenye matumizi hivyo wakati utakapofika wa kuwa na familia Nguvu zimeshakwisha hamtaweza kujenga. Nimefanya ‘Revenge’ ile waliyofanyiwa timu zingine za wanaume”. Amesema Rais Samia.

Rais Samia pia amewataka mawakala wa Mpira wa Miguu nchini waendelee kuwatangaza na kuwasemea Twiga Stars ulimwenguni ili kuwafungulia milango ya kufahamika.

“Kuna taarifa nazisikia kwa mbali kuwa FIFA wameanza kuulizia utaratibu tunaowafanyia hawa Watoto wa Twiga Stars na wanafuatilia namna tunavyowasaidia kufahamika ili waendelee kushinda zaidi, nawaomba sana msiwachukulie uwanamke wao mkawasahau, hawa wametutoa kidedea.” Amesema Rais Samia.

Awali Waziri wa Michezo, Sanaa na Utamaduni Innocent Bashungwa akizungumza kuhusiana na kuanzisha Shule za Michezo nchini, amesema kwa sasa Wizara yake kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu wameandaa shule 56 ikiwa ni vituo viwili katika kila mkoa Tanzania, na kituo kikubwa na kitaifa kinatarajiwa kujengwa wilayani Kwimba mkoani Mwanza.

Amesema Wizara pia kwa kushirikiana na Baraza la Michezo na vyombo vya usalama wanaandaa mpango mkakati wa sera ya michezo utakaokua unasimamia michezo aina 5 ambayo ni ya kipaombele nchini Tanzania.

Kwa upande wake raisi wa TFF Wallace Karia ametaja changamoto kubwa zinazowakabili kuwa ni gharama za vipimo vya afya kikiwemo cha UVIKO 19 kila wanapotaka kwenda nje pamoja na kipimo cha MRI ambacho kinapima umri wa mchezaji, hivyo kuomba changamoto hizi ziangaliwe na Serikali.

Wafamasia 2,646 kusajiliwa
Mbaroni akifanya mapenzi na Mbuzi