Timu ya taifa ya wanawake ya Tanzania (Twiga Stars) hii leo inashuka dimbani mjini Younde kumenyana na wenyeji, Cameroon katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki.

Twiga Stars ilioondoka Dar es Salaam juzi na kikosi cha wachezaji 17 na viongozi sita kwa ndege ya Shirika la Ndege la Kenya (KQ) ikipitia Nairobi, Kenya.

Afisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas alisema jana kwamba Twiga Stars wapo huko kwa mwaliko wa wenyeji wao, Cameroon ambao ni waandaaji wa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wanawake mwaka 2016.

Lucas alisema Cameroon ambao wameamua kuipa heshima Tanzania na kuona kuwa timu hiyo ina ubora  na kwamba inafaa kuipimana ubavu kabla ya kuanza kwa fainali hizo Novemba 19, mwaka huu.

Twiga Stars ambayo sehemu kubwa ya kikosi hicho kinaundwa na wachezaji wa timu ya taifa ya Wanawake ya Tanzania Bara yaani Kilimanjaro Queens ina rekodi nzuri ya kuwa kinara wa viwango vya ubora kwa nchi za Afrika Mashariki na kati lakini zaidi ni mabinga wapya wa ukanda huo – ubingwa uliopatikana Septemba, mwaka huu huko Uganda.

Rekodi hizo zimesukuma Shirikisho la Mpira wa Miguu la Cameroon (FECAFOOT) – nyumbani kwa Rais wa CAF, Issa Hayatou kuikubali Twiga Stars na hivyo kuomba kucheza nayo mwishoni mwa wiki hii. Twiga Stars iko chini chini ya Makocha Sebastian Nkoma na Wasaidizi wake Edna Lema na El Uterry Mohrery.

Kikosi cha Twiga Stars wamo makipa, Fatma Omari na Najiat Abbas; mabeki ni Wema Richard, Sophia Mwasikili, Anastasia Katunzi, Maimuna Hamisi, Fatuma Issa, Happiness Mwaipaja na Mary Masatu wakati viungo ni Donisia Minja, Stumai Abdallah, Amina Ally, Anna Mwaisura na Fadila Kigarawa ilhali washambuliaji ni Fatuma Swalehe, Asha Rashid na Mwanahamisi Omari.

Video: Obama amkaribisha Trump 'White House'
Stefano Pioli Adhihirisha Mahaba Yake Inter Milan