Tume ya Huru ya Usimamizi wa Uchaguzi nchini Nigeria – INEC, imemtangaza mgombea wa chama Tawala, Bola Tinubu (70), kuwa mshindi wa kiti cha Urais kufuatia uchaguzi mkuu uliofanyika Jumamosi ya Februari 25, 2023.
Tinubu ambaye ni Mwanasiasa mkongwe na Gavana wa zamani wa Lagos, ametangazwa mshindi baada ya kupata kura 8,794,726 ambazo ni sawa na asilimia 36 na kuwabwaga wapinzani wake wawili wa karibu Atiku Abubakar ambaye amewahi kuwa Makamu wa Rais na Gavana wa zamani wa jimbo la Anambra, Peter Obi.
hata hivyo wagombea hao wawili wametangaza kuyakataa matokeo hayo ya Urais na kutaka uchaguzi huo ufutwe na ufanyike upya wakiituhumu Tume ya Uchaguzi ya Nigeria kwa kushindwa kushughulikia changamoto kadhaa zilizojitokeza ikiwemo upakiaji wa matokeo katika mfumo wa mtandao.
Mshindi wa kiti cha Urais wa nchi hiyo, alitakiwa kupata asilimia 25 ya kura zote zilizopigwa katika majimbo 24 kati ya 36 na endapo mshindi asingepatikana uchanguzi ungeingia katika duru ya pili baada ya siku 21 kati ya mshindi wa kwanza na wa pili.