Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Suleiman Jafo ameeleza sababu zilizopelekea Chama Cha Mapinduzi (CCM) kushinda kwa asilimia 99.7 katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Novemba 24, 2019.

Waziri Jafo ameeleza kuwa katika maeneo mengi kulikuwa na mgombea mmoja wa chama hicho aliyepita bila kupingwa kwa sababu vyama vingine havikuweka mgombea, waliokuwa wameomba waliwekewa mapingamizi na kwenye maeneo mengine vyama vya upinzani kuwaondolea udhamini wagombea wao.

Katika uchaguzi huo, kwa mujibu wa matokeo rasmi yaliyotangazwa na TAMISEMI, CCM ilishinda kwa wastani wa asilimia 99.77, lakini imeshinda kwa asilimia 100 katika viti 4,263 vya mitaa.

Pia, CCM imeshinda kwa asilimia 99.9, baada ya wagombea wake kutangazwa kuwa washindi wa nafasi za uenyekiti wa vijiji 12,260 ikiacha kiti kimoja tu.

“Katika wajumbe wa mitaa, CCM imeshinda viti 114,925 ambayo ni sawa na asilimia 99.9 ya nafasi zote,” alisema Waziri Jafo.

Kwa mujibu wa takwimu rasimi, kulikuwa na nafasi 332,160 za kugombea ikiwa ni pamoja na nafasi 12,262 za wenyeviti wa vijiji, nafasi 4263 za wenyeviti wa mitaa, 63,992 za mijini, nafasi 106,622 za viti maalum kwa wanawake na wajumbe mchanganyiko 145,021.

Waziri alieleza kuwa katika uchaguzi wa mwaka huu, watu 19,681,259 walijiandikisha kupiga kura ikiwa ni kiwacho cha chini kidogo ya malengo ambayo yalikuwa watu 22,916,412.

Imeonesha kuwa wanawake walikuwa wengi zaidi (10,151,267) huku wanaume waliojiandikisha kupiga kura wakiwa 9,529,992.

Watanzania 200 huambukizwa VVU kila siku
Bibi wa miaka 75 abakwa, auawa