Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi ameutaka Uongozi wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam, Taasisi ya Sayansi za Bahari (IMS), Kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kufanya kazi ya kuielimisha jamii dhana na dhamira ya Uchumi wa Buluu.
Rais Mwinyi ametoa wito hii leo Novemba 14, 2022 wakati aliposhiriki katika Mahafali ya 52 Duru ya nne, ya Taasisi ya Sayansi za Bahari (IMS), Kampasi ya Buyu Mkoa wa Mjini Magharibi na kusema upo umuhimu wa Uongozi wa Chuo hicho kufanya kazi ya ziada ya kuelimisha jamii juu ya suala hilo na dhamira ya Serikali ya kuweka kipaumbele katika matumizi ya rasilimali za Bahari.
Amesema, Serikali itaendelea kutoa ushirikiano na IMS katika kuimarisha sekta ya Uchumi wa Buluu unaozihusisha sekta za Uvuvi pamoja na Kilimo cha Mwani kwa kuamini kuwa hiyo ndio njia bora kuibua watalamu na kwamba inatambua mchango mkubwa wa Taasisi za Elimu ya Juu na uwepo wa IMS ambao ni fursa muhimu katika maendeleo sekta ya uchumi wa Buluu.
Aidha, Rais Mwinyi pia amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa IMS katika uimarishani wa zao la Mwani, lenye kuzalisha ajira kwa kiwango kikubwa, hususani kwa akinamama na kutumia fursa hiyo kuahidi kwa Uongozi wa Chuo hicho kuwa itaijumujuisha barabara iendayo Chuo Kikuu katika mradi wa ujenzi wa barabara za Ndani.