Na Allawi Kaboyo – Bukoba.
Mkuu wa mkoa Kagera Brigedia Jenerali Marco Gaguti amewataka wakazi wa mkoa huo kagera kujikita katika kufanya mazoezi ya viungo ili kujiepusha na magonjwa yanayoitesa jamii hasa Kisukari, Shinikizo la damu na kuongezeka uzito usiokuwa rafiki kwa afya.
Gaguti ametoa ushauri huo wakati wa hafla ya uzinduzi wa kituo kipya cha mazoezi (GYM) kinachomilikiwa na kampuni ya TRS kilichopo manispaa ya Bukoba ambapo amewataka wananchi hao kuwa na mazoea ya kufanya mazoezi ili kuimarisha afya zao na kuweza kujiepusha na maradhi yanayowasumbua wananchi wengi.
Amesema uwepo wa kituo hicho utachochea maendeleo katika mkoa wa Kagera kutokana na mkoa huo kupakana na nchi 4 za Afrika Mashariki, kwa kuwa wageni watakapokuwa wanaingia nchini watapata sehemu sahihi ya kufanyia mazoezi na kuingiza fedha za kigeni.
“ Niwaombe wanakagera wenzangu tufanye mazoezi kwa ajili ya kuimarisha afya zetu, mimi ni mdau mkubwa wa mazoezi na nitakuwa nakuja hapa kufanya mazoezi,” amesema Gaguti.
Aidha ameongeza kuwa pamoja na uwepo wa kituo hicho cha mazoezi pia watanzania na wageni watapa fursa ya kunywa kahawa ya TANICA inayozalishwa mkoani humo na kupelekea kuitangaza kahawa hiyo kitaifa na kimataifa huku akibainisha faida mbalimbali za unywaji wa kahawa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa kituo hicho Evance Kamenge amesema kuwa uwepo wa kituo hicho basi uwe sababu ya kupunguza magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwa wakazi wa Kagera kwa kuwa kituoni hapo wapo wataalamu wa afya.