Katika kukabiliana na matukio ya uhalifu ambayo hufanyifanyika kutokana na ukuaji wa Sayansi na Teknolojia, Jeshi la Polisi nchini limekuja na mkakati mpya wa mafunzo yatakayowapa umahili wapelelezi wake ikiwemo matakwa ya kisheria na mambo ya msingi ya kuzingatia katika hatua za awali za upelelezi.
Hayo yamebainishwa na Mkurungezi wa makosa ya jinai nchini, Kamishina wa Polisi, Ramadhan Kingai katika shule ya Polisi Tanzania – CCP iliyopo Moshi Mkoani kilimanjaro wakati akifungua mafunzo ya siku tano ya kuwapa uwezo na umahiri wapelelezi wa Jeshi la Polisi ikiwemo washiriki kujifunza na kujadili masuala mbalimbali.
Amesema, lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wapelelezi kukabiliana na makosa ya kifedha ambapo amedai kuwa makosa mengi kwa sasa yanatendeka kwa teknolojia ya hali ya juu na kuwaomba washiriki kuyapokea mafunzo hayo kwa kujikita zaidi kujifunza ili nakupata mbinu mpya.
“Kukua kwa sayansi na teknolojia kumepelekea watu wasio waadilifu kufanya uhalifu, na katika hili Jeshi la Polisi halitawafumbia macho wahalifu hao, hivyo katika mafunzo haya watajifunza kuhusu taratibu za ukusanyaji wa ushahidi, mpango wa upelelezi na dhana nzima ya utaifishaji na urejeshaji wa mali zinazotokana na uhalifu,” amefafanua Kingai.
Kwa upande wake, Mkuu kitengo cha upelelezi wa makosa ya kifedha kutoka kutoka makao makuu ya Jeshi hilo, Kamishina Msaidizi wa Mwandamizi wa Polisi, Charles Ulaya amesema pia watajifunza namna ya kupambana na uhalifu na wahalifu.
Amesema, wahalifu siku zote wamekuwa wakipanga mbinu mpya na kwamba Jeshi hilo lipo
mstari wa mbele kuhakikisha linakabiliana na wahalifu hao, ambao wanarudisha nyuma maendeleo ya Nchi.