Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Alhamisi, Juni 17, 2021 amekagua mradi wa ujenzi wa daraja jipya la Tanzanite (New Selander) jijini Dar es Salaam na amesema kwamba ameridhishwa na kasi ya maendeleo ya mradi huo ambao umefikia asilimia 83.5.
Daraja hilo lina urefu wa kilomita 1.03 na upana wa mita 20.5, litagharimu sh. bilioni 243.75 na unatarajiwa kukamilika Desemba 14, mwaka huu.
Amesema Watanzania wanaofanyakazi katika mradi huo wahakikishe wanafanyakazi kwa umakini ili mradi utakapokamilika waweze kuwa na uwezo wa kujenga wenyewe daraja kama hilo.
“Tuhakikishe kila mmoja anakuwa mahiri katika fani yake kama ni kuchanganya zege au kusuka nondo,” amesema Majaliwa
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale alisema mradi wa ujenzi wa daraja hilo kwa sasa upo katika hatua za ukamilishwaji wa eneo la juu na tayari mkandarasi ameshalipwa shilingi bilioni 175.4.