Kampuni ya Geita Gold Mining Limited – GGML, imesambaza tani 23 za alizeti katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Halmashauri ya Mji wa Geita kwa lengo la kuleta mabadiliko katika sekta ya kilimo na jamii ya wakulima zaidi ya 5,875 wanaozunguka mgodi huo.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi mbegu za hizo kwa wakulima wa Kijiji cha Kasota Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Meneja mwandamizi wa GGML anayeshughulikia mahusiano, Gilbert Mworia alisema Kampuni hiyo imetumia Sh. milioni 108 kununua alizeti, ili kuwanufaisha wakulima 5,875 kutoka Halmashauri zote za Mji na Wilaya ya Geita.
Amesema, msaada huo unatokana na programu maalum ya kuwajengea wakulima uwezo, ikiwa ni sehemu ya mipango ya Mgodi huo wa Mazingira ya Kijamii na Kiutawala (ESG), ili kutoa elimu na mbinu bora kwa wakulima wadogo ambapo kupitia mpango huo kulianzishwa kilimo cha alizeti kwa msaada wa kitaalamu kutoka Taasisi ya Kilimo ya Cholima, shirika la utafiti wa kilimo na GGML.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Geita, Kanali Boniphace Maghembe aliipongeza GGML kwa msaada huo na kuwataka wakulima wa Geita kutumia kikamilifu kipindi hiki cha mvua na kusema “tuna jukumu kubwa la kuwahimiza wakulima wetu kutumia mbinu za kisasa za kilimo kwa sababu kinaweza kubadilisha uchumi wetu kwa urahisi.
Aidha, mmoja wa wakulima wa alizeti katika Kijiji hicho cha Kasota, Saa Kumi Makungu ambaye pia Mwenyekiti wa chama cha ushirika cha NYABUSAKAMA alisema wataboresha mavuno yao na kusema zao la alizeti halikuwepo Kasota hadi mwaka 2015 ulipoanzishwa mpango wa pamoja wa kujenga uwezo kati ya GGML na Taasisi ya Kilimo ya Cholima.
Kampuni ya AngloGold Ashanti – Geita Gold Mining Limited GGML imesaidia NYABUSAKAMA kupata mashine mbili za kiwanda cha kuzalisha mafuta zenye uwezo wa kusindika mbegu za alizeti kwa kasi kubwa ambapo mashine moja husindika mmea wa alizeti ili kupata mbegu na mashine ya pili husindika mbegu ili kupata mafuta ya alizeti kama zao la mwisho mchakato ambao huchukua dakika 25 kwa kilo 600 za mbegu za alizeti.