Bodi ya usimamizi wa Stakabadhi za ghala – WRRB, imetoa wito kwa madalali kuacha tabia ya kuwarubuni wakulima na badala yake kuwaacha waingie kwenye mfumo wa Stakabadhi ghalani ili kuuza mazao yao kulingana na bei iliyopo sokoni.

Kauli hiyo, imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa WRRB, Asangye Bangu wakati akielezea utekelezaji wa shughuli mbalimbali za bodi hiyo hii leo Februari 15, 2023 jijini Dodoma na kusema kumekuwa na wimbi la watu kwenda mashambani kwa wakulima na kuwadalalia mazao na kununua kwa bei ya chini kitu ambacho kinadidimiza maendeleo ya wakulima.

“Natoa wito kwa madalali waache kuwarubuni wakulima wawaache wajiunge katika Mfumo wa Stakabadhi ghalani ili waweze kuuza mazao yao kwa bei ya ushindani iliyopo sokoni kwa kuendelea kuuza mazao shambani inaendelea kuwadidimiza wakulima kwa sababu madalali wengi wananunua mazao kwa bei ya chini tofauti kabisa na bei iliyopo kwenye mfumo,”amesema Bangu.

Mkurugenzi Mtendaji, Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala – WRRB, Asangye Bangu.

Amesema, mafanikio yaliyopatikana baada ya kuanzishwa kwa Mfumo wa Stakabadhi za Ghalamni pamoja na ongezeko la bei za mazao, mapato ya mkulima na mapato ya Serikali kwa wastani wa asilimia 200% kutokana na urasimishaji, ongezeko la uzalishaji wa mazao kwa wastani wa asilimia 12% kwa mwaka,kichecheo cha ubora wa mazao yanayofikishwa sokoni,

Aidha, Bangu ametaja mafanikio mengine ni upatikanaji wa takwimu sahihi za mazao yanayopita kwenye Mfumo wa Stakabadhi za Ghala, ongezeko la mapato ya uhakika kwa Serikali Kuu na Serikali Mitaa na kukuza huduma za fedha vijijini,kufanikisha uanzishaji wa Soko la Bidhaa Tanzania.

“Katika zao la Korosho mara baada ya kuanzishwa kwa Mfumo palikuwa na ongezeko la asilimia 164% la bei kutoka Ths 350.00 msimu wa 2006/07 hadi kufikia Tsh 925.00 msimu wa 2007/08 mwaka wa kuanza wa Mfumo, miaka nane tokea kuanzishwa kwa Mfumo 2007/08 hadi 2014/15 wastani wa ongezeko la bei kwa mwaka ulikuwa 25% kulinganisha na ongezeko la bei miaka minane kabla ya kuanzishwa kwa Mfumo la 12% kwa mwaka kaunzia mwaka 1998/99 hadi 2006/07,” amebainisha Bangu.

Aidha, Mkurugenzi huyo amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa Mfumo 2007/08 hadi 2020/21 ukuaji wa uzalishaji umekuwa ukiongezeka kwa wastani wa 12% kwa mwaka ikilinganishwa na ukuaji wa 2% kwa mwaka kabla ya kuanzishwa kwa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala.

Wateule wa Rais Samia wala kiapo Ikulu
Ukuzaji sekta ya Kilimo, GGML yasambaza tani 23 za mbegu