Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima anatafutwa na Jeshi la Polisi Kanda ya Dar es Salaam ikiwa ni siku chache baada ya kusambaa sauti yake akimsema ‘vibaya’ Rais mstaafu, Jakaya Kikwete japo hakumtaja jina.

Jana, Polisi waliweka kambi nje ya geti la askofu huyo kuanzia majira ya saa tatu asubuhi hadi saa kumi jioni wakitavizia kumtia nguvuni bila mafanikio.

Gwajima alitoa kauli tata kanisani kwake hivi karibuni akimshauri Rais John Magufuli kukihama Chama Cha Mapinduzi endapo kile alichoeleza kuwa ni mbinu za kutaka kumnyima uenyekiti wa chama hicho zitawekwa mezani.

Katika kipande cha sauti kilichoonekana mtandaoni, Gwajima alieleza kuwa amebaini wapo watu wanaozunguka nchi nzima wakiwashawishi wajumbe wa CCM kuhakikisha wanawaunga mkono kupitisha hoja ya Rais asiwe mwenyekiti wa chama.

Alisema kuwa watu hao walimfuata hata yeye wakitaka awasaidie lakini alikataa.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Simon Siro aliwaambia waandishi wa habari kuwa Jeshi hilo linamuhitaji Gwajima kwa sababu wamepata mkanda wa video unaomuonesha akizungumza maneno ya kichochezi, hivyo wanataka athibitishe kama aliyoyasema anayaelewa.

“Tumepata clip (mkanda) inayosemekama ni ya kwake. Tunamtaka athibitishe kama hayo maneno ni ya kwake. Na kama ni yeye ameyasema, anaelewa nini kuhusu kile alichokizungumza kwa sababu hayo maneno ni ya kichochezi. Tupo kwenye uchunguzi,” Kamanda Siro anakaririwa.

Hii ni mara ya pili ndani ya kipindi cha miezi 16, ambapo Jeshi la Polisi limefika katika nyumba ya askofu Gwajima kwa lengo la kumkamata bila mafanikio. Gwajima anaendelea na kesi dhidi yake katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Dar es Salaam akituhumiwa kwa kushindwa kuhifadhi silaha ipasavyo na kumtolea lugha za kuudhi, Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo

 

Video: Ray C akamatwa na Polisi, ashindwa kuwatambua kisa ‘Unga’
Video: Seif awasha moto CCM, AFP wamtaka jaji Mutungi aifute CUF - Magazeti Juni 17 2016