Waziri wa Nishati, January Makamba amemuagiza Meneja wa Tanesco Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Grace Ntungi kuhakikisha ndani ya wiki mbili kuanzia Julai 18 2022 wale wote waliotuma maombi ya kuunganishiwa umeme wapatiwe huduma hiyo.
Waziri Makamba, ameyasema hayo wakati akizungumza na Wananchi wa Kata ya Kagongwa Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga baada ya kuwepo kwa kero za kuchelewa kuunganishiwa umeme huku wakiwa wamekamilisha hatua zote stahiki za Shirika.
“Ndani ya wiki mbili, Wale wote wenye maombi ya Umeme na wamekamilisha vigezo vyote wawe wameunganishiwa umeme. Kwa sasa vifaa vipo hivyo Sitaki kusikia Kagongwa bado wana shida ya umeme,” amesema Waziri Makamba.
Kufuatia agizo hilo, Meneja wa Tanesco Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Grace Ntungi amesema kuanzia wiki ijayo wataanza kuongeza transforma kwenye maeneo maeneo ambayo hayajafikiwa na huduma ya umeme, na kwamba tayari wameanza tafiti na kuahidi kufikia Julai, 26, 2022 watakua wametimiza agizo hilo.
Katika hatua nyingine, Waziri Makamba ameahidi kupeleka umeme kwenye migodi ya wachimbaji wadogo katika Kijiji cha Wisolele ifikapo mwezi Oktoba mwaka huu, ikiwa ni utekelezaji wa moja ya vipaumbele vya Wizara ya Nishati katika kupeleka umeme kwenye maeneo ya uzalishaji.
Ahadi hiyo ya Makamba, ameitoa wakati akiwa Wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga, baada ya kufika katika eneo hilo na kujionea shughuli za uchimbaji na uchenjuaji madini na kupokea malalamiko ya wachimbaji waliodai kutumia gharama kubwa za mafuta kuendesha mitambo.
“Baada ya kujua mahitaji ya umeme katika maeneo kama haya tukaweka mpango wa kuleta umeme kwenye maeneo ya uzalishaji ikiwamo migodi na Wisolele, mpango wa manunuzi upo hatua ya mwisho na tunatarajia mwisho wa mwezi huu tutamtangaza mkandarasi atakayeleta umeme hapa,” amesisitiza Waziri huyo wa Nishati.