Rais wa Malawi, Lazarus Chakwera amesema imani za kishirikina na upotoshaji ni miongoni mwa mambo yanayokwamisha ukuaji wa maendeleo ya teknolojia barani Afrika na kwamba ni lazima tamaduni hizo ziachwe, ili kufikia malengo chanya.
Rais Chakwera ameyabainisha hayo wakati akihutubia mkutano wa Transform Afrika uliofanyika nchini Zimbabwe akiwalenga watu wanaoshikilia imani potofu kuhusu ukuaji wa teknolojia barani Afrika, akisema wakati umefika kwa Afrika kukumbatia mabadiliko ya kuteknolojia.
Rais wa Malawi, Lazarus Chakwera, akihutubia mkutano wa Transform Afrika uliofanyika nchini Zimbabwe. Picha na Ikulu ya Malawi.
Amesema, “matokeo ya ucheleweshaji huu ni kwamba Afrika imeachwa nyuma, tumeachwa nyuma katika sekta ya kilimo na sekta nyingine nyingi. Na ukweli ni kwamba naweza kuwaambia kuwa Afrika imeachwa nyuma sana na huenda tusiwafikie wengine ikiwa tutaendelea kutumia njia zilezile za wenzetu ambao kwa sasa wametuacha mbali sana kwa miaka kimaendeleo.”
Awali, Rais wa Zimbabwe, Emmerson Munangagwa alisema ni lazima nchi za Afrika zitumie vizuri rasilimali ilizonazo kwa kujibidiisha katika masuala ya matumizi ua teknolojia, ili kurahisisha na kuharakisha maendeleo.
Rais wa Zimbabwe, Emmerson Munangagwa. Picha ya News 24.
“Ushirikiano ni muhimu kwa bara la Afrika kusonga mbele na kujenga uwezo wa sayansi na teknolojia. Hivyohivyo ni lazima tuhuishe suala la sayansi na teknolojia kwa kuwa na ubunifu na mikakati ya malengo ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya bara la Afrika,” amesema Munangagwa.