Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilaya ya Iringa Vijijini mkoani Iringa wametakiwa kuwalinda wanachama wa CCM ambao ni wapiga kura wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, Wabunge pamoja na Madiwani katika kata zote za wilaya ya Iringa Vijijini.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa UVCCM wilaya ya Iringa Vijijini, Mapesah Makala wakati akizungumza na Wajumbe wa Baraza la UVCCM Kata ya Nyang’oro kwa lengo la kutoa elimu kwa Vijana hao kuhakikisha wanatoa ulinzi kwa wanachama hasa nyakati za uchaguzi.
“Nasikia kuna watu wanafanya vitendo vya uvunjifu wa amani huku Isimani, mambo haya ni ukiukwaji wa Sheria za nchi yetu nasema wajitathimini upya huu ni wakati wa kazi na siyo kuvunja taratibu za nchi na kuleta usumbufu kwa wanachama wetu,”amesema Makala
Aidha, amewataka viongozi wa umoja huo kushiriki katika matukio mbalimbali ya kijamii ili kuunga mkono juhudi za wananchi za kupeleka maendeleo vijijini, pamoja na kuandaa vijana wenye tabia nzuri kwa jamii ili baadaye waweze kuwa viongozi bora.
Kwa upande wake Katibu wa UVCCM wilaya ya Iringa Vijijini, Julius Simalenga amewakumbusha wajumbe wa baraza hilo kufanya vikao vya kikanuni na vile vya dharura pamoja na kufanya ziara ili kujua uhai wa jumuiya ya Vijana pamoja na chama kwa ujumla.
Hata hivyo, wajumbe walioshiriki katika baraza hilo wametoa salamu za pongezi kwa Mbunge wa Jimbo la Isimani na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi na Diwani wa Kata ya Nyang’oro, Myoka wakisema kuwa Viongozi hao wamekuwa mstari wa mbele katika kuwatumikia Wananchi.