Mbunge wa Kigoma Mjini kupitia Chama Cha ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe ameitaka Serikali kuhakikisha inatoa kwa haraka vitambulisho vya taifa ili kuondokana na usumbufu wanaopata wananchi wanaoishi maeneo ya mipakani  kuhusiana na uraia.

Ameyasema hayo jana bungeni jijini Dodoma wakati wa kipindi cha maswali na majibu, ambapo aliihoji Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuhusu madai ya unyanyasaji kwa wananchi hao wa mipakani na kuitaka serikali kuchukua hatua za haraka kuhuisha upatikanaji wa vitambulisho hivyo.

“Bado kuna unyanyasaji wa wananchi kuhusu uraia, kwanini Serikali isitoe vitambulisho haraka,” Zitto alihoji.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni amesema kuwa Serikali inafanyia kazi malalamiko hayo  ya wananchi na anampongeza Zitto kwa rai yake. Aliongeza kuwa nia ya Serikali ni kuhakikisha inafikia malengo ya kuwapa vitambulisho vya taifa wananchi wote wenye sifa.

Kwa sasa Bunge linaendelea jijini Dodoma ambapo Mawaziri mbalimbali wameendelea kuwasilisha makadirio ya Bajeti ya wizara zao.

JPM aagiza taasisi za Serikali kujiunga na TTCL
Pierre atimiza ahadi yake kwa DC Jokate, ashusha madawati