Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema amewapiga marufuku askari wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) na kusema kuwa hataki kuwaona wakisumbua wananchi katika eneo la Ukonga Jijini Dar es Salaam na kutaka waliohusika wachukuliwe hatua kwa kitendo walichofanya kuwapiga wananchi.

Ameyasema hayo hii leo jijini Dar es salaam alipofanya ziara ya kuwatembelea wananchi hao ambao wamelalamika kufanyiwa fujo na kupigwa na askari hao kwa siku mbili kutokana na askari mmoja kuuawa na watu wasiojulikana,

Aidha, amesema kuwa askari hao walipaswa kufanya uchunguzi kujua ni watu gani walihusika kufanya mauaji ya askari huyo na si kwenda kufanya fujo na kuwapiga wananchi pasipokuwa na sababu.

“Kama kuna askari alipatikana ameshafariki utaratibu ulikuwa uchunguzi ufanyike ili waweze kujiridhisha baada ya hapo wale ambao wangetambulika ndiyo wangechukuliwa hatua lakini kwa hili halikubaliki, kwa hiyo nasema hivi askari wote waliohusika kufanya fujo na vurugu wachukuliwe hatua za kinidhamu na huku barabarani sitaki kuona FFU yoyote anasumbua wananchi,”amesema Mjema

Hata hivyo, amewataka wananchi walioumizwa na askari hao kwa vipigo kwa siku mbili mfululizo waweze kujiorodhesha kwa majina ili wapatiwe matibabu na kusema wale ambao wamepoteza mali zao utaratibu utafanyika kuona nini kifanyike.

Ng'ombe kutoka Kenya waingizia Serikali zaidi ya mil. 200
Taa za uwanjani zaiponza Besiktas