Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ametoa msaada wa shilingi milioni 10 ili kumuwezesha, Ernest Masenga kutatua changamoto zinazomkabili.

Masenga alikuwa msanii wa muziki wa dansi ambaye sasa anasumbuliwa na maradhi ya miguu. Pia makazi anayoishi si salama yanahitaji kukarabatiwa.

Majaliwa ametoa msaada huo leo Septemba 11, 2017 katika makazi ya Waziri Mkuu Oysterbay jijini Dar Es Salaam, ambapo msaada huo baada ya kuguswa na hali ya maisha ya msanii huyo aliyemuona kupitia kipindi maalumu kilichoonyeshwa na TBC Sempemba, 5, 2017.

“Nawaomba Watanzania wenzangu tumsaidie mwezetu ili aweze kuishi vizuri kwa sababu sanaa yake imesaidia katika kuelimisha na kuburudisha umma.”

Akipokea msaada huo kwa niaba ya msanii huyo, Godfrey Nago ambaye ndiye aliyeongoza kipindi hicho cha TBC amesema atahakikisha anasimamia vizuri fedha hizo ili zitumike kama ilivyokusudiwa.

Nago amesema anamshukuru Waziri Mkuu kwa kuwaunga mkono na kutoa msaada huo kwa sababu ameonesha kwamba Serikali inawajali wananchi wake na TBC itaendelea kuwaomba wadau mbalimbali wajitokeze na kumsaidia msanii huyo.

Kwa upande wake, Mjomba wa msanii huyo, Kanuti Mloka ambaye ameiwakilisha familia amemshukuru Waziri Mkuu kwa msaada huo kwa kuwa familia imeshindwa kumsaidia Masenga kutokana hali duni ya maisha waliyonayo.

Video: IGP Sirro apokea hundi ya shilingi milioni 120 kutoka SportPesa
Serikali kudhibiti mfumuko wa bei ya mbolea nchini