Mwanafunzi wa darasa la tano, Shule ya Msingi Butwa iliyopo Mkoani Geita, Tisekwa Gamungu ametunukiwa cheti cha ushujaa na Kamishna Mstaafu wa Jeshi la Polisi kanda Maalumu ya Dar es salaam, Suleiman Kova mara baada ya kuwanusuru wanafunzi wenzake tisa kuzama katika ziwa Victoria.

Tukio hilo lilitokea siku ya jumatatu wakati wanafunzi hao wa shule ya msingi Butwa wakirudi nyumbani, ndipo mtumbwi wao ulipopigwa na mawimbi makubwa yaliyopelekea kuzama kwa mtumbwi huo.

Dar24 media imefanikiwa kuzungumza na mtoto huyo ambapo amesema kuwa baada ya mtumbwi huo kuzama aliogelea na kufanikiwa kuvuka ng’ambo ya pili, lakini baada ya kutoka aliwaona wenzie wakihangaika kujiokoa ili wasizame ndipo alipojitosa tena ndani ya maji na kuanza kuwaokoa mmoja baada ya mwingine mpaka walipotimia tisa.

Akizungumza kwa masikitiko makubwa na Dar24 media mapema hii leo jijini Dar es salaam, mara baada ya kufanya mazungumzo na kipindi cha 360 kinachorushwa na Cloudstv, Tisekwa amesema kuwa lengo lake kubwa lilikuwa ni kuwaokoa wanafunzi wote 12 lakini watatu walikuwa tayari wameshazama.

“Baada ya kuanza kuwaokoa niliwaambia wote washikilie mtumbwi, lakini wale waliozama waliachia mtumbwi wakazama ila mimi nilikuwa nataka niwaokoe wote,”amesema

Dkt. Semboja: Awataka watanzania kumuunga mkono JPM
Video: Polisi Dar es salaam wakusanya mil.304 ndani ya siku 3