Jeshi la polisi limeingilia kati tuhuma zinazomkabili Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe ambaye anadaiwa kutoa kauli za uchochezi na kuwatukana viongozi wa Serikali wakati akizungumza na hadhara katika mkutano uliofanyika katika jimbo la Kilwa kusini.
Msemaji wa jeshi la polisi Tanzania, Kamishna msaidizi polisi, Barnabas Mwakalukwa amesema hayo leo Agosti 1, 2018 pindi akizungumza na waandishi wa habari.
Ambapo amesema kuwa mara baada ya kupata ushahidi wa kutosha juu ya tuhuma hizo Zitto atatakiwa kuripoti kwa kamanda wa polisi mkoa wa Lindi.
Zitto alialikwa kutoa hotuba katika mkutano wa hadhara ulioitishwa na mbunge wa jimbo la Kilwa Kusini, Seleman Bungara maarufu kama Bwege.
Aidha leo Agosti 1, 2018 chama cha ACT Wazalendo kimetoa msimamo wake juu ya wito ulioitishwa na Waziri Kangi Lugola na kusema kuwa Zitto aendelee na majukumu yake mpaka pale Jeshi la Polisi litakapomtaka kuripoti kwani wamedai kuwa wito wa polisi ni wito kisheria na wito wa Waziri ni harakati za kisiasa.