Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Serikali haina kipingamizi na wazo la kuifanya hospitali ya rufaa ya Haydom kuwa ya kanda kwani hatua hiyo itaupunguzia mzigo Serikali.

Majaliwa amesema kuwa Serikali ya awamu ya tano ni sikivu, na kuifanya hospitali hii kuwa ya kanda ni kazi ndogo. “Kwa hiyo nitamleta Waziri wa Afya aje awaongoze kusimamia vigezo vya kuifanya hospitali hii iwe ya kanda,” amesema.

Majaliwa amesema hayo wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa kata ya Haydom kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa kata.

“Serikali haina kipingamizi na wazo lenu, cha msingi ni vigezo muhimu vifuatwe. Kwa hiyo, nitamleta Waziri wa Afya awasaidie kuangalia vigezo,” amesisitiza.

“Kama vigezo havipo, tushirikiane kuvikamilisha kwa sababu uwepo wa hospitali hii kwa hadhi ya kanda kunaisadia Serikali kutokana na nafasi yake kijiografia,” amesema Waziri Mkuu

Amesema kuwa Serikali imepokea maombi kwa ajili ya watumishi wanaotakiwa kwenye hospitali hiyo na kwamba hivi karibuni itaajiri watumishi kati ya 5,000 hadi 6,000 wa sekta ya afya peke yake. “Tumekwishaanza kuajiri, tumeanza na sekta ya elimu kwa kuajiri walimu 4,693 ambao wote ni wa fani ya sayansi. Na sekta inayofuat ni ya afya, kwa hiyo hao watumishi 90 wanaohitajika watapatikana kwenye kundi hilo hilo,” amesema.

Wakati huohuo, Balozi wa Norway nchini Tanzania, Bibi Hannamarie Kaarstad ambaye alikuwepo kwenye mkutano huo, alisema amefarijika na mchango unaotolewa na Serikali ya Tanzania kusaidia juhudi zinazofanywa na marafiki wa hospitali walioko Norway.

“Hospitali ya Haydom ni mahali thabiti ambapo mshikamano baina ya Tanzania na Norway unaweza kuonekana kwa dhahiri. Nawashukuru watumishi wa hospitali kwa moyo wao wa kujitoa kuwahudumia wananchi wa wilaya ya Mbulu na maeneo ya jirani,” amesema.

Hospitali hiyo ambayo inaendeshwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mbulu kwa ufadhili kutoka Serikali za Tanzania na Norway, ilianzishwa mwaka 1955 ikiwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 50. Hivi sasa ina uwezo wa kulaza wagonjwa 420 kwa wakati mmoja.

 

Olamide: Ningefuata wanawake nisingeweza kufanikiwa
Izzo Bizness: Dawa za kulevya zimewashusha wasanii