Mbunge wa Kigoma Mjini na Kiongozi wa Chama cha ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe ameitaka serikali kutoa takwimu sahihi kwa wananchi ili kila mmoja aweze kujua hali ya uchumi inavyokwenda nchini.
Amesema kuwa katika uchambuzi na uchunguzi ambao wamefanya wamegundua kuwa Pato la Taifa la Tanzania lilisinyaa kati ya mwezi wa April na June 2017 tofauti na Taarifa ya Serikali iliyotolewa hivi karibuni
“Hatuja tafuta takwimu zingine, hizi ni taarifa zile zile zilizotolewa na BoT na Ofisi ya Taifa ya Takwimu NBS lakini ukikokotoa utaona uchumi tulionao unasinyaa badala ya kukua na hali ikiendelea hivi mpaka June 2018 kutakuwa hakuna uchumi Tanzania,”amesema Zitto
Hata hivyo, Zitto amegusia pia takwimu za mapato yanayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) akidai kuwa nazo haziko sahihi, huku akisema ni bora ikaeleza mapato kwa idara bila kuchanganya marejesho na madeni ambayo hayajalipwa.