Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama amewahimiza vijana nchini kutumia michezo ili kuimarisha amani, upendo na mshikamano.

Waziri Mhagama ametoa kauli hiyo, wakati wa Bonanza la michezo kwa vijana lililofanyika katika shule ya Sekondari Lindi ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha wiki ya vijana nchini kuelekea kilele cha mbio za mwenge wa uhuru kwa mwaka 2019 na Kumbukizi ya Miaka 20 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa bonanza hilo ambalo vijana walikusanyika kwa lengo la kushiriki katika michezo mbalimbali, Mhagama ameeleza kuwa michezo imekuwa ikitumika kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha ushirikiano na kuwajengea vijana uzalendo.

“Kupitia michezo mnayofursa kama vijana kuendelea kuenzi falsafa za waasisi wa taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Hayati Mzee Abeid Amani Karume ambao walikuwa wazalendo kwa taifa lao na waliimarisha muungano kwa maslahi ya watanzania wote,” alisema Mhagama

Aliongeza kuwa michezo hiyo iliyowakutaisha vijana ikatumike kama sehemu ya kuwa na amani, uvumilivu na mshikamano.

“Vijana mnatakiwa kujenga taifa kwa vitendo vinavyodumisha amani, upendo na mshikamano kama ambavyo Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere alivyotujengea taifa lenye umoja,” alieleza Mhagama

Aidha Waziri Mhagama amewasihi vijana kutambua wajibu wao katika jamii na kuifanya michezo kuwa ni miongoni mwa mambo muhimu wanayopaswa kuyaendeleza katika kutekeleza mipango waliyonayo.

Pamoja na hayo amerejea ujumbe wa Mwenge wa uhuru mwaka huu ambao pia umesisitiza ushiriki wa wananchi katika uchaguzi wa Serikali za Mtaa. Amewaomba vijana kujitokeza kwa wingi na kushiriki katika uchaguzi ili waweze kupata viongozi bora kwa maendeleo ya taifa.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi amesema kuwa Bonanza hilo la michezo limejumuisha vijana kutoka sehemu mbalimbali ikiwa ni njia moja wapo ya kuwaendeleza vijana ili waweze kuimarika kiafya na kiakili.

 

Messi afunguka mapya kuhusu Neymar
Hawa Ntarejea ''msitegemee nitarudi nilipotoka''