Tanzania na Uganda zimekubaliana kuondoa vikwazo vya biashara ili kuendeleza na kuboresha ushirikiano kati ya mataifa hayo kwenye nyanja mbalimbali.
Makubaliano hayo yamefikiwa katika mkutano wa majadiliano kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax na Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza wa Uganda na Waziri anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Rebecca Kadaga uliofanyika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Katika mkutano wao, viongozi hao wamekubaliana kukamilisha michakato ya kuendeleza miundombinu ili kukamilisha barabara zinazounganisha Uganda na Tanzania, usafiri katika ziwa Victoria ambao pia utaunganisha reli ya kisasa ya SGR kwenda Uganda.
“Tumewekeana muda ili tuweze kukamilisha baadhi ya masuala kwa haraka lakini pia kuona jinsi gani pale panapo hitaji kila nchi itoe rasilimali iweze kujipanga na kuhakikisha rasilimali hizo zinapatikana kwa wakati,” alisema Dkt. Tax.
Katika mkutano huo viongozi hao wamekubaliana pia kukamilisha ujenzi wa kituo cha uokoaji Jijini Mwanza kitakachoshughulikia maafa yanayoweza kutokea katika ziwa Victoria.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza wa Uganda na Waziri anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Rebecca Kadaga amesema mkutano huo umewawezesha kukamilisha baadhi ya mambo yaliyokuwa mezani na kujipa muda hadi mwishoni mwa mwezi Julai 2023 kukamilisha machache yaliyosalia.
Amesema, wataendelea kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja ili waweze kutatua vikwazo vilivyopo katika itifaki ya soko la pamoja la forodha.