Kama tulivyoona katika sehemu ya kwanza la makala hi kuwa Bara la Afrika linajulikana ulimwenguni kwa sifa nyingi ikiwemo utajiri wa rasilimali, umaskini, ukosefu wa usalama na ufisadi na tuliona kwamba hili limefanya baadhi ya maeno kuwa maarufu kulingana na sifa mojawapo kati ya hizo chache zilizo orodheshwa na sehemu hiyo ya kwanza tulimuangalia muasisi wa Taifa la Afrika ya Kusini, Hayati Nelson Mandela maarufu kama Madiba.
Baadaye katika sehemu ya pili tukamuona Mkongwe Haile Selassie, mtawala wa Ethiopia kuanzia 1916 hadi 1974 na baadaye kuwa mfalme (1930-1974) alikuwa ni mwanachama wa mwisho wa nasaba ya Solomoni ya taifa hilo lililopo ukanda wa Afrika ya Mashariki na wakati wa utawala wake, Ethiopia ilipata mageuzi makubwa ya kielimu.
Na leo tunaangazia jambo jipya kwa kunukuu maneno yafuatayo, “Kwa mamilioni ya watu ndani na nje ya Afrika, Kwame Nkrumah ndiye Afrika na Afrika ndiyo Kwame Nkrumah, Kwa Wakoloni na Mabeberu jina la Nkrumah ni laana kwao, kwa Masetla na Walowezi jina lake ni onyo kwamba siku zao zinahesabika, kwa Waafrika wanaokandamizwa kwa ukoloni na ubeberu wa kimataifa, jina lake ni pumzi ya matumaini, nyenzo ya uhuru, ushindi, udugu na usawa kwa wote.”
Ndivyo lilivyosomeka bango moja lililopo jijini Accra, ambalo liliwekwa Ghana miaka ya 1960 wakati wa kilele cha harakati za Uhuru barani Afrika. Ghana ilipata uhuru Machi 6, 1957 chini ya Dakta Kwame Nkrumah kama Rais wa kwanza.
Dkt. Kwame Nkrumah alikuwa ni Rais wa kwanza mzawa wa Ghana na aliheshimiwa sana kwa kuliongoza taifa hilo kupata uhuru kutoka kwa wakoloni wa Uingereza.
Kwame Nkrumah anachukuliwa kama mwanzilishi wa Taifa la Ghana, akiwa ni mwana-Pan-Africanist ambaye alianzisha Umoja wa Afrika – AU, ambao zamani ulijulikana kama Umoja wa Umoja wa Afrika – OAU huku akisifika kwa kupigania uhuru wa Taifa lake bila woga.
Lakini Nkrumah hakuridhika na uhuru wa nchi yake pekee, alisema: “Uhuru wa Ghana hautakuwa na maana kama nchi zingine za Kiafrika zitaendelea kuwa chini ya Utawala wa Kikoloni”, kuonesha jinsi mwanaharakati huyu alivyokuwa tayari kujitoa mhanga kwa ukombozi wa Bara zima la Afrika.
Mwaka mmoja tu baada ya uhuru wa Ghana, Nkrumah aliitisha Mkutano wa mataifa yote ya Afrika (All African People’s Conference) mjini Accra, Desemba 1958, kuzungumzia agenda ya harakati za uhuru, namna ya kulinda uhuru unaopatikana na kuendeleza mapinduzi ya Kiafrika. Kati ya waliohudhuria, baadhi yao ndio hao waliokuja kuwa viongozi wa nchi zao kufuatia uhuru.
Hao ni pamoja na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (Tanganyika); Dakta Hastings Kamuzu Banda (Nyazaland, baadaye kuitwa Malawi); Joshua Nkomo (Southern Rhodesia/Zimbabwe), Dakta Keneth Kaunda (Northern Rhodesia/Zambia) na Patrice Emery Lumumba (Congo Leopoldville/Zaire/DRC).
Wengine walikuwa ni Amilcar Cabral (Portuguese Guinea/Guinea Bissau); Holden Robert (Angola) na Tom Mboya (Kenya) aliyewakilisha Vyama vya Wafanyakazi na ambaye pia alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Mkutano huo.
Walihudhuria pia kwa “Mwaliko maalum”, wanaharakati kutoka Zanzibar: Abeid Amani Karume (Afro-Shirazi Party – ASP) na Ali Muhsin (Zanzibar Nationalist Party – ZNP). ASP na ZNP vilikuwa na ugomvi na uhasama mkubwa wa kisera na kimaono kiwango cha kuzuia meli ya uhuru kuong’oa nanga Visiwani.
Wakati ZNP kilichokuwa cha mrengo wa siasa za Kikomunisti na kiharakati zaidi (kwa msukumo wa Abdulrahman Babu kama Katibu Mkuu) kilitaka uhuru mara moja; ASP chenye siasa za kati chini ya Karume kilitaka agenda ya uhuru iahirishwe kwa muda (kauli yake ilikuwa “Uhuru Zuia”) kikihofia ZNP kuchukua nchi.
Karume na Muhsin walipatanishwa na Nkrumah mwenyewe pamoja na Msaidizi wake George Padmore. Wawili hao wakaonywa kuepuka kuwa “Vita vya panzi” enzi hizo za harakati za uhuru. Mapatano hayo, yaliyopewa jina “The Accra Accord” kwa lengo la kuimarisha Umoja wa Kitaifa, ulikuwa “Mwafaka” wa kwanza kwa Siasa za mpasuko Zanzibar, japo haukudumu, ambapo leo uhasama huu umerithiwa na “CCM Zanzibar” na “CUF Zanbar” kwa misingi ile ile ya kale.
Nkrumah alikuwa Mwasisi wa wazo la kuundwa kwa Shirikisho la nchi za Afrika, wazo lililozaa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU, sasa AU). Lengo lilikuwa ni kuona Afrika inajizatiti katika kujenga uchumi huru na imara; kujitegemea na kuunda Jeshi kubwa, imara kuweza kukabiliana na uvamizi kutoka nje na ambalo lingetumika pia kwa harakati za ukombozi wa Afrika.
Ni kwa njia ipi na muundo upi Shirikisho la Afrika lingefikiwa, Nkrumah na Nyerere, majabali wawili wa Siasa za Afrika enzi hizo, walitofautiana. Wakati Nkrumah alitaka Afrika iungane mara moja bila kuchelewa kabla viongozi hawajaanza kunogewa na kulewa madaraka, Nyerere alitaka Muungano wa Afrika uanze kwa awamu na kikanda, kwa nchi chache kuungana kabla ya kufikia Muungano wa Afrika nzima.
Kwenye Mkutano wa Pili wa OAU mjini Cairo, Julai 1964, Nyerere na Nkrumah walishambuliana kwa maneno na ukinzani wa hoja nusura washikane mashati juu ya hilo, ugomvi uliopewa jina “The Great Encounter” (Pambano Kuu) ambapo hoja ya Nyerere ilishinda.
Afrika na Dunia nzima bado inajiuliza, ni yupi kati ya wawili hao alikuwa sahihi juu ya kufikia Shirikisho/Umoja wa Afrika, hasa tunaposhudia kwamba hadi leo, Afrika imeshindwa kuungana, huku miungano/jumuiya za Kikanda zikiibuka na kuvunjika haraka na kirahisi? Ni nani huyu, Mwanaharakati Kwame Nkrumah, mwenye kustahili kuitwa “Baba wa Uhuru” barani Afrika, jabali la siasa aliyeweza kusuguana mabega na Mwalimu Nyerere?
Chama cha kwanza cha kiharakati nchini Ghana kilianzishwa mwaka 1947, kikiitwa “The United Gold Coast Convention” (UGCC) chini ya Dakta Joseph Danquah, kilichoanza na hoja ya kubadili jina la nchi kutoka “Gold Coast” kuwa “Ghana” kabla hata ya uhuru.
Kilimwajiri Dakta Nkrumah kama Katibu Mkuu ili kukipa nguvu, kwa kumwita kutoka Marekani na Uingereza alikoishi kwa miaka 12 na kujipatia shahada za juu katika uchumi, Sosholojia na falsafa na wakati akiwa ng’ambo, Nkrumah alijikita katika kuwaunganisha watu weusi ugenini wajitambue na watambue haki zao na kusaidia uhuru wa Afrika.
Ni Nkrumah na Weusi wengine wa nchi za Kikarebia, aliyeitisha Mkutano mkuu wa Kwanza wa watu Weusi duniani (Pan-Africanism Conference) mjini Manchester, mwaka 1945 kuzungumzia Mshikamano wa mtu mweusi.
Mwaka 1949, Nkrumah na Danquah walifarakana; Nkrumah akajiengua UGCC na kuanzisha Chama cha siasa za mrengo wa Ki-Karl Marx (Kikomunisti) cha ”Convention People’s Party” (CPP) ambapo mwaka 1951, alishitakiwa na kufungwa miezi sita kwa makosa ya “uchochezi”, akaendelea kupigania uhuru akiwa kifungoni.
Katika uchaguzi wa kwanza mwaka huo, ambapo aligombea akiwa jela, chama chake CPP, kilipata viti 34 kati ya viti 38 vya Baraza la Kutunga Sheria (LEGCO) na GCP cha Danquah kiliambulia viti vinne na Nkrumah mwenyewe katika Jimbo la Accra alipata kura 20,780 kati ya kura 23,122 zilizopigwa; mpinzani wake kutoka GCP alipata kura 2,342.
Habari za ushindi huo zilimfikia Nkrumah akiwa jela Februari 12, 1951; naye Gavana wa nchi hiyo, Aden Clarke, akalazimika kumtoa kifungoni siku hiyo na kumwomba aunde Serikali ya Mpito. na ilipofika Julai 1953, huku akionesha dhahiri kupoteza subira, Nkrumah alishinikiza kuundwa kwa Serikali yenye madaraka kamili “bila kuchelewa”.
Itaendelea sehemu ya pili …………………………………………….