Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Dkt. Issessanda Kaniki amesema baada ufuatiliaji wa mbinu za utafiti na vipimo ndani ya siku 42 tumeweza kuudhibiti ugonjwa huo hivyo hadi sasa hakuna Mgonjwa hata mmoja.
Dkt. Kaniki ambaye alikuwa akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Kagera, amesema, “baada ya Ufuatiliaji lakini pia na mbinu mbalimbali za Utafiti Mkoa wa Kagera pamoja na Nchi tunazopakana nazo kwa sasa mlipuko wa Ugonjwa wa Marburg haupo tena.”
Uchunguzi huo wa Kiikolojia utakaofanyika kati ya Juni 12 – 24, 2023 utahusisha uchukuaji wa sampuli za Wanyamapori, wanyama wa kufugwa pamoja na kufanya utafiti shirikishi jamii katika Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, Muleba na Kyerwa.
Aidha uchunguzi huo utawajumuisha Wataalamu kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Ofisi ya Waziri Mkuu ( Menejimenti ya Maafa), Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Afya, Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili, Taasisi ya Utafiti wa Wanyama Pori (TAWIRI), na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI).