Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM Bara), Christina Mndeme ametoa wito kwa Serikali na Waajiri wote nchini kuhakikisha wanachangia katika Mfuko huo wa WCF, bila kuchelewa.
Mndeme, ameyasema hayo ofisini kwake Makao Makuu ya CCM jijini Dodoma, na kusema ni wajibu wa mwajiri kuhakikisha achangia mfuko huo, kwani kutokufanya hivyo
kunawaumiza wafanyakazi.
“Nitumie fursa hii kuwaomba waajiri wote Serikalini na sekta binafsi kupeleka kwa wakati michango ya wafanyakazi, maana wote tumewekewa uwiano sawa sekta binafsi na Serikali,” amesisitiza Mndeme.
Amesema, Rais Samia kwa mapenzi mema na wafanyakazi ameamua kupunguza riba katika bajeti ya fedha 2022/2023 hadi kufikia asilimia 0.5 na hivyo kutoa unafuu kwa waajiri na hivyo hakuna sababu ya kuchelewesha michango hiyo katika mfuko wa WCF.
Ujumbe huo wa Mndeme, ameutoa mara baada ya kupokea cheti cha Usajili wa Mwajiri
kwa niaba ya Chama cha Mapinduzi CCM, kutoka Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na watu wenye Ulemavu.
Aidha, Naibu Katibu Mkuu huyo ametoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, Samia Suluhu Hassan kwa kupunguza riba kwa
wafanyakazi na waajiri hadi kufikia 0.5%.
Mfuko huo, unaohusika na fidia kwa wafanyakazi pindi wapatapo magonjwa au ajali kazini.