Waasi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati wameripotiwa kufanya unyama wa ubakaji wa halaiki katika kijiji cha Kiriwiri, Kaskazini Magharibi mwa nchi hiyo.

Shirika la msaada wa matibabu la Medicins Sans Frontieres (MSF) limesema kwamba tukio hilo lilitokea mwezi uliopita na kwamba wameweza kuwatibu wahanga 10.

MSF limeiambia Reuters kuwa wanawake wengi waliobakwa kwa pamoja na kundi hilo la waasi walivamia kijiji hicho Februari 17 walishindwa kwenda hospitali iliyo karibu kwa kuhofiwa kushambuliwa tena na kwamba walikaa wiki mbili kabla ya kufikiwa na huduma ya shirika hilo.

“Kulikuwa na hali mbaya sana. Wengine walikuwa wamepoteza fahamu kutokana na hofu na wengine walishindwa hata kueleza nini kilichotokea. Wanawake wengine walikuwa na majeraha yaliyotokana na kukatwa na mapanga,” Soulemane Amoine, mhudumu wa MSF alisimulia.

Hata hivyo, MSF haikutaja kundi linalodaiwa kuhusika na uovu huo dhidi ya wanawake.

Kutokana na matukio hayo na mauaji yanayofanywa na vikundi vya waasi, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeongeza nguvu ya vikosi vya walinda amani nchini humo kutoka 12,000 hadi 13,000 kwa lengo la kuwalinda wananchi.

Vikosi vya UN kwa kushirikiana na Serikali wanawasaka waasi katika maeneo mbalimbali, hususan maeneo ya mbali na miji.

Uasi uliibuka katika vuguvugu la kidini la mwaka 2013 ambapo baadhi ya makundi yalitangaza vita ya kidini na mengine vita ya madaraka. Aliyekuwa rais wa nchi hiyo, ya Rais Francois Bozize alilazimika kuachia madaraka na baadaye kukimbilia uhamishoni.

Tanzania yaibuka kidedea huduma za fedha jumuishi
Video: Msimamo wa Tundu Lissu akirejea nchini.